Kiungo Kimoja (01) Cha Muhimu Kitakachokuza Ustawi Wako Katika Ujasiriamali.

Kuna kiungo kimoja cha muhimu ambacho hakuna mjasiriamali yeyote anayeweza kufanikiwa bila ya  kuwa nacho.Na kiungo hicho ndicho  kimekuwa msingi mkubwa na imara kwa mafanikio aidha iwe katika maisha,biashara, na hata ujasiriamali. Na kiungo hicho si  kingine bali ni Elimu!!.

Elimu ni kiungo cha muhimu sana ambacho kila mjasiriamali anapaswa kuwa nacho na kukizingatia.Dhana inayojengeka miongoni mwa jamii kuwa ujasiriamali ni swala la kipaji cha kuzaliwa ,kurithi,au kujulikana pasi na elimu ni dhana potofu inayowakwamisha wale wanaotaka kuchukua hatua kuufanyia kazi ujasiriamali.Elimu katika ujasiriamali ni  kitu cha muhimu sana. Na kwa kusema hivyo haina maana kwamba unapaswa kurudi darasani ikiwa hukufanikiwa kupata elimu iliyo rasmi. Hapana!!. Kuna njia kadha wa kadha za kupata elimu.Elimu inaweza  kupatikana kwa kupitia uzoefu wako au kwa kupitia uzoefu wa wengine.Na kwa kuibuka kwa teknolojia ya habari na mawasiliano kwa namna moja ama  nyingine imefanya iwe rahisi kwetu kuweza kujifunza kwa kupitia uzoefu wa wengine kwa kutumia vitabu,kusikiliza CD n.k.

Kila mjasiriamali anapaswa kuwa na uzoefu na Elimu. Na kukosekana kwa vitu hivyo viwili ambayo ni uzoefu na elimu basi  kwa namna moja au nyingine kunaweza  kupeleka kutokufanikiwa au kutokudumu kwa mjasiriamali katika uwanja huu  wa biashara na ujasiliamali.

Mchakato mzima wa mjasiriamali kwa kiasi kikubwa unahusu Elimu,yaani pale tu unapojiingiza katika ujasiriamali ndio siku ya kwanza kwa wewe kuanza kujifunza.Masuala yote muhimu katika biashara na ujasiriamali kama vile utafutaji masoko na uuzaji ni masuala ambayo yanahitaji Elimu.kutafuta masoko kunahitaji kujifunza namna masoko yanavyofanya kazi kwa kujaribu njia kadha wa kadha. Na katika uuzaji unahitaji kujifunza kuhusiana na matendo, nyendo au mienendo ya watu,na jinsi wanavyofanya maamuzi ili kuweza kuja huduma,suluhisho, au bidhaa itakayokidhi haja zao.Viungo vyote hivyo ni viungo ambavyo kila mjasiriamali anapaswa kujifunza na kuviendeleza ili kuweza kuwa mjasiriamali bora na mwenye mafanikio.Elimu ni mchakato wenye  mwanzo na usiokuwa na mwisho.

Kila mjasiriamali hana budi kujiwekea lengo la kujiendeleza katika maeneo ya biashara anayoifanya.ila wengi wetu kwa kwa kutokulitambua hili tumekuwa tukifanya biashara zetu kimazoea .Tumekuwa tukifanya mambo yetu kimazoea ili tupate hela ya kula.Ni  muhimu tukajiendeleza kielimu ili kupata habari zitakazoongeza uelewa wetu katika kile tunachokifanya.

Unahitaji kuwa na ujuzi na uzoefu wa kuendesha biashara na ujasiriamali ili kuweza kufanikiwa. Wekeza sana katika Elimu ya biashara na ujasiriamali.jisajili katika kozi, makongamano, na semina za uendeshaji wa biashara Pia soma sana vitabu vya kujiendeleza ili kukuza ufahamu wako.

Hakuna kipindi kigumu katika biashara na ujasiriamali kama miaka ya mwanzo ya kuanzishwa kwake.Ni katika kipindi hicho ndipo ambapo wengi wetu  hukata tamaa hasa wakati wanapoona mambo yakienda ndivyo sivyo, yaani vile ambavyo hawakutarajia wala kutegemea.Mafanikio katika biashara na ujasiriamali sio jambo rahisi bali ni suala linalohitaji muda,juhudi, jitihada,uwekezaji wa kutosha,na kujifunza kila iitwapo Leo.Wekeza sana katika elimu.

Nakutakia utekelezaji mwema kwa kile ulichojifunza. Na Kamwe usisite kuwaalika na wenzako ili nao waweze kujipatia mambo haya mazuri yenye kuelimisha na kuhamasisha.

Geofrey Mwakatika.
Mwakatikageofrey@gmail.com.

Mchango Wa Ukuaji KIroho Katika Mafanikio, Na Mambo Muhimu Ya Kuzingatia.

Kwa kupitia maandiko,Yesu alipata kusema "utafuteni kwanza ufalme wa mungu na mengine yote mtazidishiwa". Wakati alipoulizwa ufalme wa mungu unapatikana vipi,yesu alijibu " ufalme wa mungu upo ndani yenu". Na kuna nukuu fulani isemayo kwamba "vyovyote vile mtu ajionavyo nafsini mwake ndivyo atakavyokuwa".Wakati alipoulizwa ni amri ipi iliyo kuu, yesu alijibu :" mpende bwana mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote,na kwa akili zako zote.Hii ndiyo  amri iliyo kuu,tena ni ya kwanza ". Kama ukitafakari kwa kina maana ya maneno hayo.Kulingana na yesu, amri kuu kuliko zote ilihusisha zaidi kile kilichoko moyoni,ndani ya roho zetu;hushughulikia kile kilichoko ndani yetu na wala sio kuhusu matendo yetu ya nje,japo yawe mazuri kiasi gani.

Ni matuaini yangu sote tunataka kufanikiwa. Sote tunapenda kufanikiwa. Tunaishi katika ulimwengu wa habari na taarifa.Na kwa maana hiyo, tuna kila taarifa tunazohitaji kuwa nazo ili tuweze kufanikiwa.Kwa kupitia vitabu,tovuti majalida,magazeti na njia kadha wa kadha imefanya iwe rahisi kwetu kujifunza kuhusiana na biashara, mafanikio, fedha, na uwekezaji. Lakini licha ya wingi wa  taarifa na habari tulizonazo, bado suala la mafanikio limebakia kuwa ni suala la watu wachache, yaani ni watu wachache pekee ndio ufanikiwa. Hivi ulishawahi kujiuliza, ni nini hasa kinachopeleka kufanikiwa na kutokufanikiwa kwa wengi licha ya taarifa na habari tulizonazo?.

Katika kujifunza kwangu kwa kupitia vitabu na watu kadha wa kadha nimekuja kugundua na kutambua kwamba; mafanikio katika nyanja yoyote ile kwa kiasi kikubwa huwa yanachangiwa na ukuaji wa kiroho.Hatua ya kwanza na ya msingi katika mafanikio ni ukuaji kiroho.

Sote tunafahamu kuwa ili tuweze kufanikiwa iwe katika maisha au biashara basi tunahitaji kuwa na uvumilivu,kutokukata tamaa,kuwa waaminifu,waadilifu,na wachapa kazi n.k.Ila kile wasichokitambua wengi ni kwamba, mambo yote hayo ni matunda ya roho. Kuna nukuu fulani katika biblia isemayo kwamba ”tunda la roho ni upendo,furaha,amani,uvumilivu,utu wema,fadhili,uaminifu,upole,na kiasi”.

Mafanikio yoyote yale katika maisha huwa yanaanzia ndani.Ni kupitia ndani yako, ndani ya roho yako ndipo unapofanikiwa kuwa mwenye imani, mwenye kujiamini,kuwa mtulivu, kutokuwa na shaka,kutambua unachopenda kufanya,kutambua kipaji chako,na hata kutambua dhumuni la maisha yako. Ila wengi wetu kwa kutokutambua hili, tumekuwa tukitumia muda na nguvu zetu nyingi katika kujishughulisha na hali zetu za nje.Na baadhi ya hali hizo ni kama vile kuweka akiba,uwekezaj n.k .Na kwa kusema hivyo haina maana kuwa haupaswi kufanya uwekezaji.Hapana!.kufanya uwekezaji ni jambo la muhimu sana tena sana kwa wewe kulifanya.lakini kama utafanya uwekezaji huo huku moyoni ukiwa ni mwenye mashaka ya kupoteza,kutokujiamini n.k,basi kaa na ujue kwamba ni lazima utapoteza, kwani vile ujionavyo nafsini mwako ndivyo utakavyokuwa.

Badiliko lolote lile la maisha huwa linaanzia ndani.Mafanikio yanaanzia ndani yako.Bila badiliko la fikra pamoja na nafsi kamwe haitowezekana kufanikiwa.Na kwa maana hiyo kabla haujafikiria kufanya uwekezaji wowote ule wa nje ni muhimu kwanza ukazingatia kuwekeza ndani yako.

Kwa kweli kuna mchango mkubwa sana tena sana wa ukuaji kiroho katika mafanikio. Ukuaji kiroho ni jambo la muhimu sana na linalopaswa kuzingatiwa na kila mmoja wetu.Sasa basi ikiwa utachukua hatua katika kuwekeza kwenye kukua kiroho, hapa kuna mambo machache unayoweza kuanza kuyafanya na yakawa na mchango mkubwa sana katika safari yako ya kukua kiroho. Na baadhi ya mambo hayo ni kama yafuatayo..

1. Thamini uhusiano wako na mungu.
Hakuna jambo lililo jema na lililo bora kama kuthamini uhusiano wako na mungu. Kwa kupitia vitabu kadha wa kadha vya kidini kama vile Quran na Biblia, amri kuu na iliyo kubwa ni kumpenda mungu juu ya yote.Na kwamba upendo wetu kwake unajengwa kwa kumsikiliza yeye na kuwasiliana naye kila iitwapo leo.Na baadhi ya njia unazoweza kuzitumia katika kuthamini uhusiano wako na Mungu ni kwa kupitia maombi,sala,tahajudi n.k

2. Lisha ubongo wako kwa mawazo mazuri.
Moja ya njia muhimu unayoweza kuitumia katika kukua kiroho ni kuulisha ubongo wako kwa mawazo mazuri yenye kuelimisha, kuhamasisha, na kukujenga. Wekeza sana muda wako katika kusoma vitabu kadha wa kadha vilivyo vizuri ambavyo kwa namna moja au  nyingine vitaweza kukupatia nguvu,hamasa,na motisha.Na vitabu kama vile biblia ,Quran, Tao tae ching n.k, ni vitabu vyenye hekima na maarifa mazuri sana ndani yake. Na kwa kufanya hivyo kwa namna moja au nyingine kutakusaidia sana katika kukua kiroho.

3.Jali Mahitaji Ya Wengine.
katika moja ya maandiko yake,Paulo alipata kusema " Msitende neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno;bali kwa unyenyekevu,kila mtu na amhesabu mwenzie kuwa ni bora  kuliko nafsi yake.Kila mtu asiangalie nafsi yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine ".ili kuweza kukua kiroho basi litakuwa ni jambo jema kama utajifunza jinsi ya kuyajali mahitaji  ya wengine. Ni muhimu tuwapende,tuwahudumie,na kuwajali wengine.

4. Tenga muda kila siku katika kuwa peke yako na kukaa kimya.
Moja ya nidhamu ambayo kila mmoja wetu anapaswa kujijengea ni ile nidhamu ya kutenga angalau saa moja katika kuwa peke yako na kukaa kimya.Kwa kujijengea nidhamu hii itakufanya kuweza kuwa mtu  mtulivu na makini, mvumilivu,kuondokana na mihemko,kupata mawazo mbalimbali yaliyo bora na mapya yatakayokufanya kuwa mbunifu katika kazi ama shughuli zako n.k. Hii ni moja ya nidhamu muhimu sana  ambayo kila mmoja wetu anapaswa kuizingatia.Na unaweza ukatumia muda huo katika kufanya tafakari au tahajudi.

Nakutakia utekelezaji mwema kwa kile ulichojifunza. Na Kamwe usisite kuwaalika na wenzako ili nao waweze kujipatia mambo haya mazuri yenye kuelimisha na kuhamasisha.

 Geofrey mwakatika
mwakatikageofrey@gmail.com

Sababu 5 Za Wengi Kutokuinuka Kiuchumi, Na Mambo Muhimu Ya Kufanya Ili Kuondokana Nazo.

Habari yako rafiki?.Moja ya shauku walionayo watu wengi iwe katika maisha au biashara ni kutaka kufanikiwa. Kutaka kupata mafanikio yawe ya kiuchumi,kiafya, ki-uhusiano, kifedha,na hata kiroho ni moja ya malengo yanayotamaniwa na kila mmoja wetu.Lakini licha ya uwepo wa nia,shauku,na juhudi tunazoziweka ili kuweza kuyafanikisha  malengo hayo bado mambo yetu yanaonekana hayasongi. Kuna sababu kadha wa kadha zinazopeleka wengi kushindwa kufanikiwa kaika maeneo hayo,ila katika makala yetu ya leo tutaangalia na kujifunza sababu zinazopeleka wengi kutofanikiwa kuinuka kiuchumi.Hivi umekwishawahi kujiuliza, ni sababu gani zinazowafanya wengi wasiinuke kiuchumi? .kuna sababu kadha wa kadha za wengi kutoikuinuka kiuchumi.Na baadhi ya sababu hizo ni kama zifuatazo.

1.Kukosekana kwa maarifa.
Kuna nukuu fulani katika biblia isemayo kwamba “ watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa”.Msingi namba moja wa mafanikio katika nyanja yoyote ile kaika maisha ni maarifa.Maarifa ni ile njia inayotumiwa katika kujitoa katika shida ama kuweza kupata kitu au hekima.Na kukosekana huko kwa maarifa miongoni mwa watu wengi ndiko kwa kiasi kikubwa hupeleka wengi kutokuinuka kiuchumi. Na kwa maana hiyo, ili kuweza kufanikiwa katika nyanja yoyote ile katika maisha unahiaji kwanza kuwa na maarifa.Na maarifa hayo yanaweza kupatikana kwa kutumia njia kadha wa kadha kama vile kujisomea vitabu,kuwa na mshauri, kuhudhuria semina n.k.Kwa kujipatia kwako maarifa kwa namna moja au nyingine kutakusaidia katika kufungua hazina zilizositilika kichwani mwako na ambazo ikiwa zitatumika kimadhubuti basi zinaweza kukuinua kibinadamu,kiuchumi,ki-uhusiano, na kiroho.

2.Kutokutumia maarifa tuliyonayo.
Hakuna jambo lililo gumu katika maisha kama nidhamu binafsi.nidhamu binafsi ni ile hali a kujiwezesha kufanya kile unachopaswa kufanya hata kama haujisikii kufanya.Wengi wetu tunajua kile tunachopaswa kufanya ila kwa namna moja ama nyingine  tunashindwa kufanya.Kujipatia kwako maarifa na kisha kutokufanyia kazi maarifa ulionayo ni sawa na kazi bure.Mafanikio katika maisha huwa hayategemei sana kiasi cha elimu au fedha ulizonazo. Mafanikio katika maisha huwa yanategemea uharaka wa kujipatia maarifa mapya mazuri na wepesi wa kuyatumia.ila wengi wetu kwa kutokulitambua hili tumekuwa tukikazana katika kujiongeza maarifa bila ya kuwa na utahayari wa kuyatumia maarifa hayo.Kuna nukuu fulani katika biblia isemayo kwamba” jiangalieni basi jinsi msikiavo;kwa kuwa mwenye kitu atapewa,na yule asiyekuwa na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anachodhaniwa kuwa nacho”.Na nukuu hiyo ina maana kwamba; kubali kujipatia maarifa ,yatumie kuwanufaisha wengine,usipoyatumia yatayeyuka. Ni muhimu ukajipatia maarifa na kuyatumia maarifa hayo.

3. Matumizi mabaya ya muda.
Kila mmoja wetu ana masaa ishirini na nne kwa siku,na jinsi unavyoyatumia masaa hayo ndiko kunakoweza kuleta kufanikiwa au kushindwa kwako.Muda ni rasiliamli ya muhimu sana.Muda ni rasiliamli ya pekee isiyoweza kurudi wakati inapotumika. Swali la muhimu unalopaswa kujiuliza ni kwamba; je,unautumia vipi muda wako?.uwekezaji wowote unaoufanya sasa kwa kutumia muda ulionao ndio utakachokuja kuvuna kesho.kamwe usikubali kutumia muda wako vibaya kwa kutokuwa na hiki au kile.Anza na matumizi mazuri ya muda pamoja na akili yako,na mungu atafungua njia ya kile usichonacho sasa. Ila wengi wetu kwa kutokulitambua hili tumekuwa tukiutumia muda wetu katika mambo kadha wa kadha ambayo kwa namna  moja au nyingine yanakuwa hayana manufaa kwetu.

4. Matumizi mabaya ya pesa.
Moja ya elimu ya muhimu sana na inayopaswa kuzingatiwa na kila mmoja wetu ni elimu ya fedha. Na kwa bahati mbaya elimu hii huwa haifundishwi darasani.Kukosekana kwa elimu ya misingi ya fedha ndio kunakosababisha wengi kuwa na matumizi mabaya ya pesa.Tatizo tulilonalo wengi sio upatikanaji wa fedha bali ni usimamizi bora wa fedha.Kupata fedha ni jambo rahisi kwani fedha huwa inapatikana kulingana na kiasi cha thamani unachokitoa kwa wengine.ili uwe huru kifedha, ondoa au punguza kero za mahitaji ya wengine.Na kwa kufanya hivyo watu watakupa pesa zao na utakuwa huru kukamilisha mahitaji yako yote.  lakini licha ya hilo, suala la kusimamia kimadhubuti kile tunachokipata bado limekuwa ni tatizo. Kukosekana kwa usimamizi mzuri wa fedha ndiko kunakosababisha wengi wetu kutokuinuka kiuchumi kutokana na uwepo wa matumizi mabaya ya pesa.Ni muhimu tukajifunza jinsi ya kusimamia na kutumia fedha zetu vizuri.

5. Kutafuta pesa ndio lengo la kwanza.
Kama nilivyosema hapo awali kwamba: ili uweze kuwa huru kifedha, basi ondoa au punguza kero za mahitaji ya wengine. na kwa kufanya hivyo watu watakupa pesa zao na utakuwa huru kukamilisha mahitaji yako yote.ila wengi wetu kwa kutambua ama kutokutambua tumekuwa tukiiweka fedha kuwa lengo letu la kwanza.Na katika kujifunza kwangu kuhusiana na maendeleo binafsi nilichokuja kujifunza ni kwamba; utajiri ni kupata unachokitaka na umaskini ni kukosa unachokitaka.Ukipenda kuhudumia watu kwanza utainuka haraka.maarifa ya kupenda kuhudumia watu yatakuwezesha kuona kile ambacho wengine hawaoni.Yatakuwezesha kuona majibu na kero za watu.Na utatumia maarifa hayo katika ubunifu wa mbinu na huduma mpya.

Nakutakia utekelezaji mwema kwa kile ulichojifunza. Na Kamwe usisite kuwaalika na wenzako ili nao waweze kujipatia mambo haya mazuri yenye kuelimisha na kuhamasisha.
Geofrey Mwakatika.
Mwakatikageofrey@gmail.com.

Umuhimu Wa Uandishi Na Kitu Kimoja Cha Kufanya Ili Kupata Nguvu Ya Kuandika.

Ni kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikipokea maoni kadha wa kadha kutoka kwa baadhi ya wasomaji wa mtandao huu.Na moja ya  maswali ambayo nimekuwa nikiulizwa mara kwa mara, ni namna gani naweza kuwa mwandishi? Itanichukua muda gani mpaka kuweza kuwa mwandishi? Nahitaji nini na nini ili kuwa mwandishi? Jinsi gani naweza kupata nguvu ya kuandika?. Wengi wanataka kuwa waandishi ila kwa namna moja au nyingine wanashindwa kufahamu ni wapi pa kuanzia. je,nawe pia ni mmoja wapo? Je, ungependa kuwa mwandishi ila haujui ni wapi pa kuanzia?.Na Kama jibu lako ni ndiyo, basi  nina habari nzuri na mbaya kwako. Habari mbaya ni kwamba; kuwa mwandishi  sio jambo rahisi kama wengi wetu wanavyodhani au wanavyofikiri, bali ni kazi kama zilivyo kazi zingine ambazo zinahitaji muda,kujituma, kujifunza, na  juhudi za mara kwa mara.Na habari nzuri ni kwamba; Uandishi kama zilivyo fani nyingine ni sanaa ambayo kila mtu anaweza kujifunza. Hakuna mtu anayezaliwa na kuwa mwandishi bali ni matokeo ya kujifunza na kutumia kile unachojifunza ndio huwafanya wengi kuweza kuwa waandishi.

Kwa kweli kuna manufaa makubwa sana tena sana kwa wewe kuwa mwandishi.Na kwa machache tu ni kwamba; Uandishi unasaidia katika kukuza uelewa wako kuhusiana na kile unachojifunza.Uandishi unakuza uwezo wako wa kufikiri na kutafakari.Uandishi unakupatia mawazo mapya na yaliyo bora zaidi.Uandishi unaushughulisha ubongo wako na kukufanya  kuwa uwe mwenye uzalishaji na mtulivu.Na kubwa zaidi uandishi kwa namna moja au nyingine unaweza kukupatia kipato.

Sasa basi  kama nilivyosema hapo awali kwamba; watu wengi wanataka kuwa waandishi ila kwa namna moja au nyingine wanashindwa kufahamu ni wapi pa kuanzia. Na ninaposema hivyo haina maana kwamba mimi ni bora katika Uandishi.Hapana!!, Kama wewe unaniona hivyo basi  ni sawa.ila kwa upande wangu bado najiona kuwa ni mwanafunzi ambaye kila iitwapo leo natafuta namna bora zaidi ya kujifunza zaidi na zaidi. Suala la kujifunza katika maisha ni jambo lisilokuwa na mwisho. Mara baada ya hayo naona tusiende mbali sana.Lengo kuu la makala hii ni kukushirikisha jambo moja la muhimu na la msingi unalopaswa kulifanya kila siku ili uweze kujijengea nidhamu ya Uandishi na ambalo litakupa nguvu ya kuweza kuandika.Na jambo ninalokwenda kukushirikisha ni kitu ambacho binafsi huwa nafanya kila siku.

Moja ya falsafa zangu katika maisha ni kujifunza kila siku .Na nikiwa katika harakati zangu za kujifunza nilipata nafasi ya kusoma vitabu kadha wa kadha kuhusiana na Uandishi. Na baadhi ya vitabu hivyo ni the artist's way, Bird by bird, na  on becoming a writer. Ukiachilia mbali vitabu hivyo ni kupitia kitabu cha the artist way kilichoandikwa na julia cameroon ndipo ambapo nilipopata falsafa moja ya msingi sana na ambayo ndiyo imekuwa muhimili mkubwa wa shughuli zangu za kiuandishi.

Julia Cameron, kupitia kitabu chake cha the artist way anatupatia mbinu na kitu muhimu sana cha  kufanya ili kuweza kuwa mwandishi bora na kuweza pia kupata nguvu ya kuandika.Na mbinu hiyo si nyingine bali ni kuandika kurasa tatu kila siku asubuhi kwa muda wa wiki 13.Hii ni changamoto kubwa sana lakini inalipa.

Na mpaka hapo unaweza ukawa unajiuliza kwamba, ni nini hasa ninachoweza kuandika wakati ndo kwanza nataka kuanza kujifunza kuhusiana na Uandishi?. Hilo ni swali zuri sana. Na unachotakiwa kufanya hapa ni kuandika kitu chochote tu kile kitakachopita mawazoni mwako.kwa mfano;  kama unawaza kwamba haujui cha kuandika ,basi  chukua karatasi na uandike neno " sijui cha kuandika ". Na urudie kuandika neno ilo bila kupumzika mpaka uhakikishe umefanikiwa kuandika kurasa tatu.Na wakati utakapofanikiwa kukamilisha kurasa hizo unaweza kuendelea na mambo yako.Hiyo ni changamoto unayoipaswa kuifanya kwa muda wa wiki 13 bila ya kukosa hata siku moja.kwa kweli utapata manufaa makubwa sana tena sana kama matokeo ya kufanyia  kazi zoezi hili.Na baadhi ya manufaa utakayoyapata ni kama niliyoyaorodhesha hapo awali.Chukua hatua sasa na ufanyie kazi kile ulichojifunza.Nakutakia utekelezaji mwema na tupo pamoja.

Geofrey mwakatika
mwakatikageofrey@gmail.com